Wanawake watumishi wa Taasisi ya Tiba Mifupa Muhimbili (MOI)

Dar es Salaam, 06/03/2019. Wanawake watumishi wa Taasisi ya Tiba Mifupa Muhimbi (MOI) leo wametoa msaada wa kijamii wenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 4 kwa Watoto wenye vichwa vikubwa na Mgongo wazi wanaopata matibabu MOI pamoja na Watoto wenye Saratani wanaopata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Msaada huo umetolewa kutokana na michango ya wanawake wote ambao ni watumishi wa MOI ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani tarehe 08/03/2019.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amewapongeza wanawake wa MOI kwa kuamua kusherehekea siku ya wanawake duniani mwaka 2019 kwa kutoa msaada wa kijamii jambo ambalo ni la kuigwa na kupongezwa.

“Nawapongeza sana kwa uamuzi wenu huu adhimu, hii inaonyesha ni namna gani mna moyo wa upendo kwa wagonjwa hususani Watoto. Mkiwa jeshi kubwa zaidi ndani ya Taasisi, sisi viongozi wenu tunaunga mkono jitihada zenu kubwa, Pia tunaheshimu na kuthamni kazi kubwa mnayoifanya” Alisema Dkt. Boniface

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi MOI Bi. Regina Alexanda ameushukuru Uongozi wa MOI kwa kutambua na kuheshimu kazi kubwa inayofanywa na wanawake ndani ya Taasisi ikiwa wao ndio wengi kuliko watumishi wanaume.

“Tunashukuru kwamba Uongozi unatambua, unaheshimu na kuthamini mchango wetu katika maendeleo ya Taasisi ndio mana Mkurugenzi Mtendaji wetu Dkt.Resopicious Boniface pamoja na majukumu mengi aliyonayo amejumuika nasi leo, pia amekuwa akituunga mkono katika mambo mbalimbali tunamini ataendelea hivyo” Alisema Bi Regina

Umoja wa watumishi wanawake MOI unahusisha watumishi kutoka kada zote ikiwemo madaktari na Wauguzi ambapo msaada huu wa kijamii kwa wagonjwa umelenga kuhamasisha jamii kutoa msaada kwa wale wenye mahitaji maalum hususani wagonjwa na Watoto.