MOI na Peking zaendesha kambi ya upasuaji

Madaktari Bingwa wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu leo wameshirikiana na madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking cha nchini China kufanya upasuaji mkubwa  wa kuondoa uvimbe kwenye Ubongo, upasuaji wa kuviba mishipa ya damu iliyopasuka kwenye ubongo pamoja na upasuaji wa mgongo

Upasuaji huu umefuatia ujio wa jopo la madaktari bingwa watatu wa upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya chuo Kikuu cha Peking cha china ambao walipokelewa MOI tarehe 23/02/2019

Akizungumza katika chumba cha Upasuaji MOI, Dkt Nicephorus Rutabansibwa amesema ushirikiano kati ya MOI na Peking utakuwa wenye manufaa makubwa kwani huduma za MOI zitaendelea kuwa bora na watanzania wataendelea kupata huduma hizo hapa nchini billa ya kwenda nje ya nchi.

“huu ni muendelezo wa ushirikiano tulioingia na wenzetu hawa wa Peking mwaka jana, tunaamini tutabadilishana uzoefu na wenzetu hawa ambao wamepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya matibabu, kupitaia ushirikiano huu mbinu tunazopata zitatusaidia kuendelea kutoa tiba bora na kwa wakati kwa wagonjwa wetu” alisema Dkt Rutabansibwa

Dkt Rutabansibwa amesema leo watawafanyia upasuaji wagonjwa 3 mmoja atafanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia darubini ya kisasa, mwingine upasuaji wa mgongo na mwingine atafanyiwa upasuaji wa kuziba mishipa ya damu iliyopasuka kwenye kichwa.

Pia amesema ujio huu wa wataalamu kutoka peking umelenga kuweka mazingira bora ya ushirikiano na MOI ili watakapo kuja tena wajue ni maeneo gani yanahitaji kuwa kipaumbele kwenye ushirikiano.

Kwa upande wake kiongozi wa jopo la madaktari bingwa kutoka Peking Peking amesema ushirikiano kati ya MOI na Peking utakuwa wenye mafanikio makubwa na utawanufaisha wagonjwa pamoja na madaktari vijana ambao watapata fursa ya kusoma kenye chuo chao

“Tumefarijika kuja Tanzania, tumewaeleza hali halisi ya hospitali yet una vifaa tulivyonavyo, tunaamini kupitia ushirikiano huu wataalamu wa hapa watajifunza na pia tutatoa fursa kwa wataalamu 2- 3 kuja kujifunza kwetu” Alisema Profesa Zhao

Kambi hii ni sehemu ya muendelezo wa mkataba wa ushirikiano uliosainiwa kati ya MOI, Chuo Kikuu cha MUHAS na Hospitali ya Peking ya China ambao umejikita katika ,Mafunzo ya muda mrefu na Mfupi, utafiti,tiba pamoja na uboreshaji wa miundombinu.