Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Taasisi ya tiba ya Mifupa MOI

Zanzibar, 31/01/2019. Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesaini mkataba na Taasisi ya tiba ya Mifupa MOI utakaowawezesha wagonjwa kutoka visiwani humo kupata matibabu ya kibingwa waliyokuwa wakiyafuata nje ya nchi kwa gharama kubwa.
Utiaji wa saini wa mkataba huo umefanywa na katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Bi Asha Ali. Abdulla pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface. Pia, tukio hilo limeshuhudiwa na Mwanasheria wa MOI Bwana Suleiman J. Mgerwa pamoja na Mwanansheria wa Wizara ya Afya Zanzibar Bi Shufaa Nassoro Ali.
Akizungumza katika tukio hilo, Bi Asha Ali Abdula amesema Serikali ya Zanzibar imeamua kurasimisha ushirikiano na Taasisi ya MOI kwani imekuwa ikitumia gharama kubwa kupeleka wagonjwa nje ya nchi wakati huduma hizo zinapatikana hapa Tanzania.
“Tumekuwa tukipeleka wagonjwa wengi nje ya nchi kwa matibabu hususani hawa wa mifupa, sasa tunafahamu kwamba wenzetu hawa wa MOI wameboresha sana huduma zao hivyo tumeamua wagonjwa wetu waende MOI badala ya kwenda nje, naamnini Mashirikiano hayo haya yatakuwa yenye tija kwa wananchi wetu” alisema Bi Asha.
Bi Asha ameongeza kwamba wagonjwa wamekuwa wakienda MOI kupata huduma kwa kipindi kirefu lakini mkataba huu unafanya ushirikiano uwe rasmi na wagonjwa wapokelewe na kupata huduma kwa namna bora zaidi.
” Hili sio jambo jipya, wagonjwa wetu wanakuja huko kupata huduma na tunashukuru kwamba mmekuwa mkiwahudumia vyema, mkataba huu utaboresha namna mnavyowapokea na hata kama kutakuwa na changamoto yoyote kwa mgonjwa tutajadiliana na kuangalia nini cha kufanya kwani mambo sasa yamekuwa rasmi” Alisema Bi Asha
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema ni heshma kubwa kwa MOI kuingia mkataba na Wizara ya Afya ya Zanzibar ikiwa ni ishara tosha kwamba Serikali ya Zanzibar imetambua maboresho yaliyofanyika MOI pamoja na huduma za ubora wa hali ya juu zinazotolewa.
” Tunawashukuru sana kwa Kuona kwamba huu ni muda muafaka wa kuingia makubaliano nasi, tunawashukuru sana kwa kutambua ubora wa huduma zetu, tunawaahidi kwamba wagonjwa watakaofika kwetu tutahakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati kama ambavyo mnatarajia” alisema Dkt Boniface
Dkt Boniface amesema kwamba huduma zinazopatikana MOI kwa sasa ni sawa na zile zinazotolewa katika mataifa yaliyoendelea hivyo wagonjwa kutoka Zanzibar watapata huduma nzuri tena kwa wakati.
” Ndugu Katibu Mkuu tumeboresha sana huduma zetu, tuna kitengo cha kisasa cha radiolojia, maabara na wodi za kisasa (Executive ) hivyo tunaamini wagonjwa kutoka Zanzibar na watanzania wataendelea kupata huduma bora” Alisema Dkt Boniface
Hatua hii ni itapelekea wagonjwa kutoka Visiwani Zanzibar kupata huduma za kibingwa katika Taasisi ya MOI na hivyo kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu.