MOI na Zydus zaanzisha ushirikiano

Dar es Salaam, Madaktari bingwa wa Taasisi ya Mifupa MOI kwa kushirikiana na madakari bingwa kutoka Hospitali ya Zydus ya nchini India leo tarehe 26/10/2018 wameendesha kliniki maalum kwa wagonjwa wenye matatizo ya Mgongo, Nyonga, Magoti, Kiwiko na Bega.
Kliniki hiyo ya ubobezi wa juu (Specialized clinic) imefanywa kufuatia tangazo lilitoka na kuwataka wagonjwa wenye matatizo tajwa wajisajili ili kuonana na mabingwa hao bila gharama yoyote.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema Taasisi ya MOI iliingia mkataba wa ushirikiano na hospitali ya Zydus na kukubaliana kushirikiana katika nyanja za tiba, utafiti, mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi pamoja na kubadilishana uzoefu.
“Kliniki hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya mkataba wetu tulioingia miezi michache iliyopita, na kwakuwa leo ndio tumeanza tumekubaliana huduma za kumuona daktari ziwe bure kabisa” alisema Dkt Boniface.
Pia, Dkt Boniface amesema zaidi ya wagonjwa 120 watapata fursa ya kukutana na madaktari bingwa wa MOI na wa hospitali ya Zydus na kupata ushauri kuhusiana na magonjwa waliyonayo.
“Tumejipanga na tunatekeleza kwa vitendo agizo la Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli la kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa nchini na hivyo kuondokana na rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi.” Alisema Dkt Boniface
Aidha, Dkt Boniface amesema kwa wale wagonjwa ambao watabainika kuhitaji upasuaji ,watapewa utaratibu na watapata huduma hiyo hapa nchini kwani kwa sasa MOI ina vifaa vya kisasa na wataalamu wabobezi sawa na mataifa mengine duniani.
Wakati huohuo Hospitali ya Zydus imemtunukia cheti cha shukrani na heshima Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface kutokana na mchango wake wa kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora wanapofika MOI.
Kwa upande mwingine, Muwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Zydus Bw. Himanshu Sharma amesema ni heshma kubwa kushirikiana na Taasisi ya MOI, Pia ni fursa kwa kukutana na madkari wa MOI na kubadilishana uzoefu.
Ninafurahi ushirikiano kati ya hospitali yetu ya Zydus na MOI unashamiri na hili ni jambo jema sana la kujivunia kwa pande zote mbili, sisi tunaahisi kuendelea kuulinda ili wagonjwa wengi zaidi wanufaike” alisema Bw. Himanshu Sharma
Taasisi ya MOI imekua ikishirikiana na Taasisi mbalimbali za kimataifa ili kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuwa bora na za kiwango cha kimataifa.