Naibu waziri wa afya Dr Ndugulile atembelea MOI

Dar es Salaam, 27/09/2018. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile leo ametembelea na kukagua hali ya utoaji wa huduma katika baadhi ya vitengo katika Taasisi ya MOI na kukagua usimikaji wa mitambo ya kisasa katika kitengo cha radiolojia yenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 5.6 .
“Lengo la ziara yangu ni kukagua maendeleo ya usimikaji wa mitambo hii ya kisasa ya MRI, CT SCAN, X-ray, Ultra sound, nimeona na kujiridhisha imekamilika kwa asilimia 99% . Naomba niwaelekeze mkamilishe mambo machache yaliyobaki ndani ya wiki hii ili wiki ijayo wagonjwa waanze kupata huduma hapa”. Alisema Dkt Ndugulile.
Pia, Dkt Ndugulile ametembelea vitengo vya mazoezi tiba pamoja na utengenezaji wa viungo bandia ambapo amekagua na kujiaonea hali ya utoaji huduma na kujiridhisha kwamba huduma zimeboreka katika kipindi cha miaka 3 ya Serikali ya awamu ya tano na kwa sasa watanzania wanapata huduma kwa wakati ijapokuwa kuna changamoto chache ambazo Serikali inazishughulikia.
Aidha, Dkt Ndugulile ameupongeza uongozi wa MOI kwa kuhakikisha usimikaji wa Mitambao unafanyika kwa wakati na hali ya utoaji huduma ni nzuri na ya kuridhisha kwani wagonjwa wamekuwa wakipata changamoto ya kwenda nje ya MOI kufuata vipimo hivyo.
Akitoa taarifa ya hali ya utoaji huduma na usimikaji wa mitambo hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amemueleza Dkt Ndugulile kwamba hali ya utoaji wa huduma ni nzuri, wagonjwa wanapata huduma stahiki kwa wakati na idadi ya wagonjwa wanaopata huduma imeongezeka maradufu baada ya eneo la kutolea huduma kuboreshwa.
“Mh Naibu Waziri, hali ya utoaji huduma katika taasisi yetu ni nzuri, idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji imeongezeka na kufikia 700-900 kwa mwezi kutoka 500 kutokana ongezeko la vyumba 2 vya upasuaji katika jengo hili, awali tulikua na vyumba 6 sasa vimekuwa 8, hii nikutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali hii ya awamu ya 5 inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli” alisema Dkt Boniface
Akihitimisha yake Dkt Ndugulile amesema ni adhma ya Serikali kuhakikisha huduma zote zinapatikana hapa nchini hivyo ni vyema kama kuna kifaa chochote kinachohitajika taarifa itolewe Wizarani ili kifaa hicho kiwekwe kwenye mpango na bajeti na kununuliwa kwani utaalamu na weledi upo wakutosha.