Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John William Herbert Kijazi atembelea MOI

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Mhandisi John William Herbert Kijazi leo tarehe 28/08/2018 amemtembelea na kumjulia hali Dkt Hamis Kigwangala ambaye anapata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI. Balozi Kijazi amepokelewa na Wakurugenzi Wakuu wa MOI na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Balozi Kijazi amempa pole Mh Dkt.Hamisi Andrea Kigwangalla na kumtakia heri na apone haraka ili aweze kurejea kwenye majukumu yake ya kila siku kwani Taifa linauhitaji mchango wake.
“Pole sana ,Mungu atajalia utapona na utarejea nyumbani mapema , na kwa kuwa wewe ni daktari ukiona hali si nzuri utawafahamisha wenzio mapema ili mjadiliane namna ya kuikabili hali itakayojitokeza” Alisema Balozi Kijazi.
Aidha, Balozi Kijazi amemueleza Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface kwamba kwa sasa wananchi wanaridhishwa na huduma zinazotolewa na MOI na Muhimbili kwa ujumla na hii ni faraja kubwa kwa Serikali na hivyo kuelekeza ari hiyo iendelezwe.
“Pamoja na Jitihada kubwa za Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli za kuboresha huduma za Afya hapa nchini, nanyi pia kwa upande wenu mnajitahidi sana na wananchi wanaridhishwa na huduma mnazotoa. Nafahamu kuna changamoto chache lakini bado mmeendelea kufanya kazi nzuri” Alisema Balozi Kijazi.
Kwa upande wake, Dkt Hamis Kigwangalla amemshukuru Balozi Kijazi kwa kumtembelea na kumjulia hali na amemueleza kwamba afya yake imeendelea kuimarika na anaamini katika kipindi kifupi kijacho madaktari watakapojiridhisha wanaweza kumpa ruhusa ya kutoka hospitalini.
“Ninaendelea vizuri, afya yangu inaimarika siku hadi siku, na pia naendelea na mazoezi na kila siku najiona imara zaidi, hii ni ishara tosha kwamba ninaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani” Alisema Dkt Kigwangalla.
Dkt Kigwangalla alihamishiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI tarehe 12/08/2018 baada ya kupata matibabu katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.